Akihutubia ujumbe wa viongozi wa kikabila kutoka mkoa wa magharibi mwa Yemen wa Ibb Alhamisi jioni, Kiongozi wa Ansarullah Sayyid Abdul-Malik Badruldeen al-Houthi amesema nchi za Kiarabu ambazo zimeanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel ndio ambazo zinaonyesha uadui na kutekeleza hujuma ya kijeshi dhidi ya Yemen. Amesema maadui wanalenga kuvuruga umoja wa Yemen lakini Wayemen watendelea katika mkono wao wa uhuru na kujitegemea na hawatawaruhusu wageni waingilie mambo yao ya ndani.
Kwingineko katika hotuba yake, Kiongozi wa harakati ya wananchi ya Ansarullah ya Yemen amesema Marekani, ikishirikiana na magaidi wakufurishaji ambao ni waitifaki wake, inajenga vituo kadhaa vya kijeshi katika mikoa ya mashariki mwa nchi hiyo ya Hadhramaut na al-Mahrah na halikadhalika mji wa Aden na pwani ya Bahari ya Sham.
Al-Houthi ameashiria ujenzi wa vituo hivyo vya kijeshi vya Marekani nchini humo na kusema Wayemen hawatakubali kupokea amri kutoka Washington. Aidha ametahadharisha kuwa maadui wanafanya juu chini kuibua mifarakano na migawanyiko baina ya watu wa Yemen.
Al Houthi amesema maadui sasa wanatumia fursa iliyojitokeza ya usiitishwaji vita unaosimamiwa na Umoja wa Mataifa kujitayarisha kwa awami nyingine ya vita kwa sababu walifeli katika miaka iliyopita.
Inafaa kuashiria kuwa, Saudia ikishirikiana na UAE na kwa himaya ya Mareakni na utawala haramu wa Israel na madola mengine ya Magharibi ilianzisha mashambulizi dhidi ya Yemen mwishoni mwa mwezi Machi 2015 kwa lengo la kuiondoa madarakani Harakati ya Ansarullah na kumrejesha usukani Abdrabbuh Mansour Hadi, rais wa zamani wa nchi hiyo aliyejiuzulu na kukimbilia Riyadh.
Vita vilivyoanzishwa na Saudi Arabia na washirika wake dhidi ya Yemen na kuendelea hadi sasa vimeshapelekea mamia ya maelfu ya watu wasio na hatia kupoteza maisha, mbali na kuwaacha mamilioni wakiwa hawana pa kuishi. Aidha vita hivyo vimesababisha matatizo mengi ya ukosefu wa chakula, matibabu na elimu kwa watu wa Yemen.
Katika kulipiza kisasi jinai hizo, Jeshi la Yemen hutekeleza mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya maeneo ya kistratijia ya Saudi Arabia na UAE.