IQNA

Mashindano ya Qur'ani ya Iran

Mashindano ya 40 ya Qur'ani Tukufu ya Iran yaanza kwa washiriki 138 kutoka mataifa 64

15:14 - December 31, 2023
Habari ID: 3478120
IQNA – Toleo la 40 la Mashindano ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu ya Iran, moja ya matukio ya kifahari na bora zaidi ya Qur'ani duniani, lilianza Jumamosi mjini Tehran kwa duru ya awali ya mchujo.

Katika duru hii, jopo la majaji katika Kituo cha Masuala ya Qur'ani cha Shirika la Wakfu na Masuala ya Hisani Iran litatathmini washindani waliotuma kanda zao za video ambapo kwa ujumla ni washiriki 138 wanaume na wanawake kutoka nchi 64.

Duru hii ya mchujo  itaendelea hadi Januari 2, 2024.

Washiriki waliofuzu wataingia katika duru kuu itakayofanyika Tehran kuanzia tarehe 15 hadi 19 Februari, sanjari na kumbukumbu ya kuzaliwa Imam Sajjad (AS), Imam wa nne wa Waislamu wa madhehebu ya Shia.

Hamid Majidimehr, mkuu wa Kituo cha Masuala ya Qur'ani cha Shirika la Wakfu na Masuala ya Hisani la Iran aliiambia IQNA Jumapili kwamba wawakilishi 300 kutoka zaidi ya nchi 100 wamejiandikisha kwa ajili ya toleo la 40 la mashindano hayo, lakini ni 138 tu kati yao waliofaulu kufika mchujo wa awali.

Alisema mashindano ya mwaka huu yatakuwa "ya ushindani na yenye changamoto" kwani baadhi ya nchi, kama vile Misri na Saudi Arabia, zimetuma washiriki wa hali ya juu.

Washiriki watachuana katika tuzo za juu katika kategoria za usomaji wa Qur'ani Tukufu (kwa wanaume) na kuhifadhi Qur'ani Tukufu na usomaji wa Tarteel (kwa wanaume na wanawake).

Mashindano ya Kimataifa ya Qur'ani ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni hafla ya kila mwaka inayoandaliwa na Shirika la Wakfu na Masuala ya Hisani la Iran, ambayo huwavutia wasomaji na wahifadhi Qur'ani Tukufu kutoka sehemu mbalimbali za dunia.

 

4190887

Habari zinazohusiana
captcha