IQNA

Ahl-ul-Bayt (AS); Taa za Mwongozo /3

Msomi: Imam Sadiq (AS) aliziinua nyanja zote za fikra za madhehebu ya Shia

19:43 - November 06, 2023
Habari ID: 3477850
TEHRAN (IQNA) – Kwa kutumia fursa iliyotolewa na hitilafu za kisiasa miongoni mwa watawala wa wakati wake, Imam Sadiq (AS) aliweza kuinua fikra za madhehebu ya Shia katika nyanja mbalimbali na katika nyanja zote za kiitikadi, amebaini mwanazuoni mmoja.

Akizungumza na IQNA, Allahridha Akbari amesema Maimamu Maasumu (AS)- wanaotoka katika kizazi kitoharifu cha Mtume Muhammad (SAW)- wote ni wafasiri, walezi na waendelezaji wa Uislamu lakini kwa sababu Hadithi nyingi zilizotufikia kutoka kwa Maasumu ni kutoka kwa Imamu Sadiq (AS) tunamchukulia Imamu wa sita kuwa ndiye muasisi wa madhehebu ya Kiislamu ya Shia.

Amesema Uimamu wa Imam Sadiq (AS) ulikwenda sambamba na uhamishaji madaraka kutoka kwa Bani Umayya kwenda kwa Bani Abbas na hivyo alitumia fursa hiyo kupandisha daraja fikra za Kishia katika nyanja mbalimbali na katika nyanja zote za kiitikadi ambapo alitoa mafunzo kwa wanafunzi mahiri na mashuhuri katika nyanja mbalimbali za fiqhi, usul, theolojia ya Kiislamu, sayansi mpya na sayansi ya majaribio.

Hata wale ambao hawakuwa Mashia, waliweza kujifunza kuhusu vipengele tofauti vya Uislamu wa Kishia kupitia kauli za Imam Sadiq (AS).

Upana wa mafundisho ya Imam Sadiq (AS) ni kwamba wengi wa wakuu au waanzilishi wa madhehebu za  Kisunni wanajiona kuwa wanafunzi wa Imam huyu wa sita katika madhehebu ya Shia.

Akbari ameongeza kuwa, kila Imam (AS) alitekeleza matakwa ya wakati ule, na ndio maana Imam Ali (AS) na Imam Hussein (AS) walianzisha makabiliano ya kijeshi na madhalimu wa wakati huo, Imam Sajjad (AS) akatoa msaada wa kijeshi, msingi wa kuinua jamii kimaanawi kwa njia ya sala na dua naye Imam Sadiq (AS) alifanya vikao vya kielimu na kiroho ili kuiongoza jamii kwenye lengo la Mwenyezi Mungu na kutetea Uislamu.

Kwa mujibu wa Hadithi kutoka kwa Imam Ali (AS): “Anapofariki Faqihi na mwanachuoni, pengo linaibuka  katika Uislamu na haliwezi kujazwa.” Kwa msingi huo iwapo mwanachuoni ana hadhi kama hiyo katika Uislamu, basi hadhi ya Imam Maasumu bila shaka iko juu zaidi..

Sheikh Allahridha Akbari anasema Imam Sadiq (AS) ana hadhi ya juu ya kielimu kutokana na nafasi yake ya kukuza na kuendeleza mafundisho ya Kiislamu katika nyanja zote.

Aidha ameongeza kuwa jamii ya Shia inapaswa kufikia kiwango katika nyanja za kisayansi na kielimu ambazo watu wengine wote watakuja kwao kupata elimu.

Sheikh Akbari  alitoa mfano wa Hadithi kutoka kwa Imam Baqir (AS) ambaye alisema, "Nenda mashariki au magharibi, lakini hautapata elimu ya kweli isipokuwa kwa kile kinachotoka kwetu, Ahl-ul-Bayt (AS)."

Kwa hiyo wale wanaotafuta elimu ya kweli waende kwa Ahl-ul-Bayt (AS) na wale wanaofuata madhehebu ya Ahl-ul-Bayt (AS) waendeleze mafundisho yao, Sheikh Akbari amesisitiza.

Kishikizo: Imam Sadiq
captcha