IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Kuna udharura wa Jihadi ya haraka ya kubainisha uhalisia wa mambo

19:06 - February 08, 2022
Habari ID: 3474906
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu leo amekutana na makamanda wa Jeshi la Anga na Kikosi cha Ulinzi wa Anga cha Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ambako amesisitiza kuwa kuna udharura wa kufanyika Jihadi ya haraka ya kueleza na kubainisha ukweli na uhalisia wa mambo.

Ofisi ya Kulinda na Kuchapisha Athari za Ayatullah Ali Khamenei imeripoti kuwa, katika kumbukumbu ya hatua ya kihistoria ya maafisa wa Jeshi la Anga ya kutangaza baia na utiifu wao kwa Imam Ruhullah Khomeini (M.A) mnano tarehe 19 mwezi Bahman mwaka 1357 (8 Februari 1979), baadhi ya makamanda na wafanyakazi wa Jeshi la Anga na Kikosi cha Ulinzi wa Anga cha Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran leo Jumanne wamekutana na kuzungumza na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei. Katika kikao hicho Ayatullah Khamenei ametaja baia hiyo kuwa ni tukio muhimu sana na la kustaajabisha na kuongeza kuwa: Leo hii, vita vya kukabiliana na uchokozi wa adui wa kupotosha ukweli, mafanikio, maendeleo na ustawi wa kustaajabisha wa Mfumo wa Kiislamu vinahitaji harakati ya kujihami na kuhujumu kwa pamoja katika fremu ya Jihadi ya kueleza na kubainisha mafanikio hayo.

Amesema kuwa, kwa hakika baia hiyo haikuwa mkono wa utiifu kwa Imam kama mtu binafsi, bali kwa malengo na maadili aliyokuwa akiwakilisha; ilikuwa baia kwa jihadi tukufu iliyokuwa ikiongozwa na Imam Khomeini. Amesisitiza kuwa harakati hiyo ya kiroho ingali inaendelea na kwamba wale wote wanaoendeleza harakati hiyo wana mchango ndani yake.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema harakati hiyo ya maafisa wa Jeshi la Anga imeonesha kuwa, mahesabu ya Marekani na utawala mbovu wa Kipahlavi yalikwenda mrama na walipata kipigo na dhoruba kutokea sehemu ambayo hawakuitarajia. 

Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa: "Iwapo vikosi vya kambi ya haki na Uislamu vitashiriki ipasavyo katika nyanja zote za jihadi, ikiwa ni pamoja na uwanja wa kijeshi, kisayansi, utafiti na nyanja nyinginezo, na kuwa na matumaini na kutoogopa ubabe wa kidhahiri wa upande wa pili, hapana shaka kuwa mahesabu ya adui yatakwenda mrama, kwa sababu hiyo ni ahadi ya Mwenyezi Mungu ambayo hapana shaka kuwa itatimia."

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema hii leo pia mahesabu ya Marekani yanakwenda visivyo na inapata pigo kutoka mahala ambako haikutarajia yaani kutoka kwa marais wawili wa nchi hiyo, rais aliyetangulia na rais wa sasa, ambao wanashirikiana kuangamiza heshima iliyosalia ya nchi hiyo.

Ayatullah Khamenei ameutaja udikteta wa vyombo vya habari kuwa ni miongoni mwa aina mbalimbali za udikteta wa madola ya Magharibi licha ya madai yao ya kutetea uhuru wa kujieleza. 

Ameashiria mifano na vielelezo vya udikteta huo wa vyombo vya habari wa madola ya Magharibi kama vile kuondolewa jina na picha ya Shahidi Qasem Soleimani katika mitandao ya kijamii na kusema: Wanazuia kuoneshwa au kuchapishwa kila neno na picha inayopinga nchi za Magharibi, na wakati huo huo mitandao hiyo ya kijamii inatumiwa kwa kiwango cha juu zaidi kuharibu sura ya Uislamu na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Mwanzoni mwa kikao hicho Ayatullah Khamenei amewataka wananchi kufuata maagizo yanayotolewa na wataalamu wa afya juu ya jinsi ya kukabiliana na maambukizi ya virusi vya corona ikiwa ni pamoja na kuvaa barakoa na kupiga chanjo ya COVID-19.  

4034793

captcha