IQNA

Bashar al Assad achaguliwa kwa wingi wa kura kuendelea kuwa rais wa Syria

17:24 - May 28, 2021
Habari ID: 3473953
TEHRAN (IQNA)- Rais nchini Syria Rais Bashar al Assad kwa mara nyingine amechaguliwa kuwa rais wa nchi hiyo na baada ya kutangazwa ushindi wake, wananchi wa maeneo mbalimbali ya Syria wamemiminika mitaani kusherehekea ushindi.

Wananchi wa Syria wamekesha katika miji mbalimbali ya nchi hiyo kufurahia ushindi mutlaki wa Rais Bashar al Assad baada ya Spika wa Bunge la nchi hiyo kutangaza kuwa, Rais Bashar al Assad ameshinda uchaguzi huo kwa asilimia 95.1 ya kura za ndani na nje ya Syria.

Hata hivyo baada ya uchaguzi mkuu wa Syria kufanyika kwa ufanisi wa hali ya juu na kujitokeza idadi kubwa ya wananchi katika uchaguzi huo, nchi za Magharibi zimezidi kuonesha udumilakuwili wao kwa kuwawekea vikwazo wananchi hao kwa sababu ya kutumia haki yao ya kidemokrasia. 

Katika duru hii ya uchaguzi Rais wa sasa Bashar al-Assad ameshindana na naibu waziri wa zamani Abdullah Sallum Abdullah ambaye ni mwanachama wa Chama cha Muungano wa Kisosholisti na Mahmoud Ahmad Marei, ambaye ni mkuu wa Shirika la Kiarabu la Haki za Binadamu. 

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Syria imeandaa uchaguzi huo kwa njia bora huku kukiwa na usalama katika aghalabu ya maeneo ya nchi hiyo. Kuhusiana na nukta hii, Mohammad Khaled al-Rahmoun amesema kulikuwa na masanduku 12,102 ya kupigia kura katika miji na maeneo yote ya Syria. Kwa hivyo kufanyika uchaguzi katika kona zote za Syria kunahesabiwa kuwa ni mafanikio muhimu kwa mfumo unaotawala Syria.

 uchaguzi wa rais nchini Syria unafanyika katika hali ambayo tokea mwaka 2011 hadi sasa nchi hii ya Kiarabu imekuwa ikikabiliwa na njama za kimataifa ambazo zinatekelezwa kupitia hujuma ya magaidi wakufurishaji watenda jinai. Njama hizo zinazoendelea zimekuwa zikitekelezwa kwa lengo la kuiangusha serikali halali ya Rais Bashar Assad. Ni kwa kuzingatia nukta hiyo ndio maana nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani zikadai kuwa uchaguzi wa sasa hauna uhalali. Propaganda hizo zimekuwa zikienezwa ili kupunguza kiwango cha ushiriki katka uchaguzi huo.

Kufanyika  uchaguzi wa rais nchini Syria kwa mara ya pili katika muongo mmoja ni baraka inayotokana na kushikamana wananchi na viongozi na jeshi la nchi hiyo sambamba na uungaji mkono wa mhimili wa muqawama. Hivi sasa serikali halali ya Syria imebakia madarakani ikiwa imara kabisa na si tu kuwa imeshavuka hatari ya kuangushwa bali imeweza kufikia uthabiti wa kisiasa. Kushiriki kwa wingi wananchi wa Syria katika upigaji kura kuna maana ya kuwepo matumaini kuhusu kurejea maisha katika hali ya kawaida na Syria kupata tena hadhi katika uga wa kieneo.

/3474822

Kishikizo: Assad syria uchaguzi
captcha