IQNA

Israel yaendeleza mauaji ya umati Ghaza, mashahidi wakaribia 2,000

19:31 - August 04, 2014
Habari ID: 1435964
Jeshi la utawala haramu wa Israel limeendeleza mauaji ya umati katika eneo la Ukanda wa Ghaza hii leo kwa siku ya 28 mtawalia na kuifanya idadi ya mashahidi wa hujuma hiyo kukaribia 2,000.

. Wizara ya Afya ya Palestina katika Ukanda wa Ghaza imetangaza kuwa, licha wa utawala katili wa Israel kutangaza leo usitishaji vita kwa muda wa masaa saba, bado umeendeleza jinai zake bila kikomo ikiwemo shambulizi dhidi ya shule ya Shirika la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina la Umoja wa Mataifa (UNRWA) katika eneo la Rafah, kusini mwa Gaza na kuua shahidi makumi ya wakimbizi waliokuwa wamekimbilia shuleni hapo ili kuokoa maisha yao.
Kwa upande wake, Msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas Sami Abu Zuhri amesema kuwa, usitishaji vita uliotangazwa na Wazayuni hii leo ni wa upande mmoja na hauna itibari yoyote kwa Wapalestina. Amebainisha wazi kwamba, Israel imetangaza usitishaji vita huo wa masaa saba kwa lengo la kuficha jinai ulizozifanya dhidi ya raia wasio na hatia katika eneo hilo la Ghaza hasa kwa kuua watoto, wanawake na watu wazima wasio na hatia. Kwa mujibu wa utawala katili wa Israel, usitishaji vita huo ungeyahusu baadhi ya maeneo ya Ukanda wa Ghaza.
Wakati huo huo, Naibu Katibu Mkuu wa Harakati ya Jihadul-Islami ya Palestina, amesema kuwa muqawama utaendelea kulinda silaha zake kwa ajili ya kukabiliana na utawala wa Kizayuni wa Israel. Ziyad Nakhalah, ameashiria njama za Wazayuni na Marekani zenye lengo la kuupokonya muqawama silaha zake katika Ukanda wa Ghaza na kusema kuwa, suala la kupokonywa silaha haliwezekani kwani silaha ni kwa ajili ya kulinda raia wa eneo hilo. Aidha ameashiria kikao cha jana cha makundi ya Kipalestina na Misri mjini Cairo, kwa ajili ya kusitisha mapigano na kuongeza kuwa kikao hicho kilikuwa na mafanikio. Amesema kuwa, kile kinachosisitizwa na Wapalestina ni kuhitimishwa mzingiro na kukomeshwa mashambulizi ya kinyama ya Wazayuni dhidi ya Ukanda wa Ghaza.
Afrika Kusini yatuma ujumbe Misri kuhusu jinai za Israel huko Ghaza
Wakati huo huo Afrika Kusini imetuma ujumbe Misri kwa shabaha ya kufanya mazungumzo na viongozi wa ngazi za juu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kuhusiana ukatili wa Israel dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Ghaza. Ujumbe huo uliotumwa na Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini umekutana na Muhammad Sabih Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu anayeshughulikia masuala ya Palestina mjini Cairo, na pande hizo mbili zimejadili suala la kusimamishwa mashambulizi ya makombora ya Israel huko Ghaza. Taarifa zinasema kuwa, ujumbe wa Afrika Kusini umesisitiza juu ya kusimamishwa mapigano na kuondoshwa kikamilifu mzingiro wa kidhuluma wa Ukanda wa Ghaza, uliodumu kwa miaka saba sasa. Ujumbe wa Afrika Kusini umetangaza kuwa tayari kuwapokea watoto wa Kipalestina waliojeruhiwa na kuwapatia matibabu zaidi kwenye  hospitali za Afrika Kusini. Hivi sasa Afrika Kusini inafanya juhudi ya kuzungumza na nchi na taasisi mbalimbali za kimataifa lengo la kupatikana njia za kukomeshwa mashambulizi ya kijeshi ya Israel huko Ghaza.
Ghaza : Shule nyingine ya UN yapigwa na makombora ya Israel
Wapalestina 10 waliuawa shahidi Jumapili tarehe 3, kutokana na mashambulizi dhidi ya shule ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Palestina, UNRWA, maeneo ya Rafah.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon amelaani vikali mauaji hayo akisema ni ukiukwaji wa sheria ya kimataifa ya kibinadamu, inayolazimu pande husika katika vita kuheshimu raia wa Palestina, wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa na majengo yake.
Ban Ki Moon ameongeza kwamba majengo ya Umoja wa Mataifa yanapaswa kuwa sehemu za usalama si za mapigano. Jeshi la utawala haramu wa Israel liliarifiwa mara nyingi kuhusu majengo hayo,  alisema, na uchunguzi unahitajika juu ya mashambulizi hayo, watekelezaji wakipaswa kuwajibika. Katibu Mkuu ameleza kusikitishwa sana na ongezeko la ghasia na mauaji ya  mamia ya Wapalestina huko Ghaza.

1435625

captcha