IQNA

Watetezi wa Qur'ani Tukufu

"Moto Hauwezi Kuchoma Jua," Waislamu wa Uholanzi wasema katika maandamano ya kutetea Qur'ani Tukufu

20:36 - August 27, 2023
Habari ID: 3477502
TEHRAN (IQNA)- Waislamu nchini Uholanzi wamefanya maandamano makubwa kulaani vitendo vya mara kwa mara vya kuvunjiwa heshima Qur’ani Tukufu nchini Uswidi na Denmark.

Waandamanaji hao walikusanyika katika barabara kuu ya The Hague Jumamosi jioni kuelezea hasira zao kuhusu vitendo vya mara kwa mara vya kuvunjia heshima Qur'ani Tukufu katika nchi za Nordic.

Waandamanaji hao, miongoni mwao wakiwamo Waislamu wa Uholanzi, Afghanistan, Iraqi, Pakistani, Uturuki na Iran, walikusanyika mbele ya Ubalozi wa Uswidi mjini The Hague huku wakiwa wameshikilia nakala za Qur’ani Tukufu mikononi mwao.

Vile vile walikuwa wameshika alama zinazosomeka, “Qur’an inatupatia nuru ya kutuongoza, moto hauwezi kuchoma Jua.”

Waandamanaji hao walishutumu serikali za Uswidi na Denmark kwa kuruhusu vitendo hivyo vya chuki dhidi ya Waislamu huku wakipaza sauti na kusema, “Acheni kuchoma kitabu chetu na vitabu vitakatifu,” na “Aibu kwa serikali za Denmark na Uswidi!”

Pia waliseoma aya za Qur'ani Tukufu wakati wa maandamano yao katika mji huo wa magharibi wa Uholanzi.

Mwishoni mwa maandamano yao, waandamanaji hao waliitaka serikali ya Uholanzi kuwasilisha mswada unaosisitiza ulinzi wa imani na kuhakikisha kuwepo kwa amani kwa makundi ya kidini na yasiyo ya kidini na watu binafsi.

Katika kipindi cha miezi kadhaa iliyopita, vitendo mbalimbali vya kuvunjia heshima Qur'ani Tukufu vimefanyika nchini Uswidi  na Denmark, ingawa nchi hizo mbili zimesema zinatafuta njia za kuzuia kisheria vitendo hivyo ili kupunguza mvutano unaoongezeka kati ya nchi za Kiislamu. .

Idara ya Mahakama ya Denmark hatimaye iliamua siku ya Ijumaa kuwasilisha mswada wa kupiga marufuku kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu kufuatia athari mbaya za hatua kama hizo, ikisema kwamba muswada huo "utakataza kuvunjiwa heshima  vitu vyenye umuhimu mkubwa wa kidini kwa jamii ya kidini."

 

3484935

Habari zinazohusiana
captcha