IQNA

Jeshi la Yemen lashambulia kiwanda cha mafuta cha Aramco Jeddah kulipiza kisasi jinai za Saudia

21:55 - March 26, 2022
Habari ID: 3475077
TEHRAN (IQNA)- Moto umeteketeza kiwanda cha mafuta cha Aramco huko Jeddah nchini Saudi Arabia, katika oparesheni za kijeshi za jeshi la Yemen na wapiganaji wa harakati ya Ansarullah wanaolipiza kisasi hujuma za muungano wa vita unaoongoza na Saudia.

Vyombo vya habari vya Saudia mapema leo Jumamosi vimechapisha picha mpya za athari za operesheni ya anga ya vikosi vya jeshi la Yemen ndani ya ardhi ya nchi hiyo, ambapo moto mkubwa unaonekana katika kituo cha mafuta cha Aramco huko Jeddah.

Mtandao wa Al-Hadath umerusha hewani moja kwa moja mkanda wa video wa kiwanda cha kusafisha mafuta cha Aramco kikiteketea kwa moto huko Jeddah, na kuripoti kuwa miale ya moto ilikuwa ikiwaka kwenye kituo hicho na kwamba moshi mweusi na mnene ulikuwa umetanda eneo hilo. 

Wakati huo huo, baadhi ya vyanzo vya habari vinaripoti kuwa Mwanamfalme wa Saudi Arabia, Mohammed bin Salman amekutana na makamanda wakuu wa kijeshi wa Saudia.

Kufuatia operesheni ya makombora ya Jeshi la Yemen dhidi ya maeneo ya Saudia na kituo cha mafuta cha Aramco huko Jeddah, vyombo vya habari vimeripoti ongezeko la bei ya mafuta duniani.

Huko Imarati, mshirika mkuu wa Saudi Arabia katika vita vyake dhidi ya taifa la Yemen, pia utawala wa nchi hiyo umejiweka katika tahadhari ya hali ya juu kwa kuhofia mashambulizii ya kilipiza kisasi kutoka Yemen.

Waziri wa Habari wa Yemen Zaifullah al-Shami ameiambia Saudi Arabia kwamba "Moto unaowaka huko Aramco ni ishara ya kuzingirwa kwa watu wa Yemen, na hakuna serikali itakayoweza kuuzima hadi mzingiro huo utakapoondolewa."

Msemaji wa Jeshi la Yemen, Brigedia Jenerali Yahya Saree, amesema vikosi vya jeshi hilo vitaendelea kushambulia vituo vya kimkakati na nyeti vya nchi wanachama wa muungano unaoongozwa na Saudi Arabia katika mashambulizi makubwa yaliyopewa jina la Operesheni ya Kuvunja Mzingiro, hadi nchi hizo zitakapokomesha mzingiro huo.

Moto wa vita uliowashwa na Saudi Arabia na washirika wake dhidi ya Yemen kuanzia mwezi Machi 2015 na kuendelea hadi sasa umeshapelekea mamia ya maelfu ya watu wasio na hatia kupoteza maisha, mbali na kuwaacha wengine zaidi milioni nne wakiwa hawana pa kuishi. 

Uchokozi na uvamzi wa kijeshi wa Saudia dhidi ya Yemen umebomoa na kuharibu zaidi ya asilimia 85 ya miundombinu ya nchi hiyo masikini zaidi katika Bara Arabu na kuisababishia pia uhaba mkubwa wa chakula na dawa nchi hiyo ya Waislamu.

4045032

captcha