IQNA

Mwanajeshi Marekani akamatwa kwa kujaribu kuua Waislamu Msikitini na kuwazika hapo

18:31 - June 11, 2016
Habari ID: 3470377
Ofisa mwenye cheo cha meja katika jeshi la Marekani amekamatwa baada kujaribu kuwaua msikitini na kuwazika hapo katika jimbo la Carolina Kaskazini.

Taarifa ya Polisi ya Kaunti ya Hoke imesema kuwa, Meja Russell Thomas Langford, kamanda huyo mwenye cheo cha meja katika jeshi la Marekani anakabiliwa na mashitaka ya kutishia kufanya mauaji, udini, kutishia umati mkubwa kwa silaha, kutoa matamshi ya kibaguzi na kuvizia. Habari zinasema kuwa, Alkhamisi iliyopita Meja Langford alitishia kuwaua kwa bastola na kuwagonga kwa gari lake, Waislamu waliokuwa wakielekea katika msikiti wa Al-Madina, katika mji wa Raeford, Kaunti ya Hoke, jimbo la Carolina Kaskazini, kutekeleza ibada ya Swala nyakati za jioni wakati huu wa mwezi mtukufu wa Ramadhani. Imearifiwa kuwa, mbali na kuwatishia kwa bunduki na kuwatolea maneno makali ya kibaguzi, ofisa huyo mwandamizi wa jeshi la Marekani alimwaga kwa makusudi na kejeli, nyama za nguruwe katika lango la kuingia msikiti huo. Ibrahim Hooper, msemaji wa Baraza la Mahusiano la Waislamu nchini Marekani amekosoa kitendo hicho na kulitaka jeshi la polisi nchini humo kuwadhaminia usalama waumini wa Kiislamu wanapotekeleza ibada zao na haswa ibada za usiku katika mwezi huu wa Ramadhani. Mwanajeshi huyo mwenye chuki dhidi ya Uislamu aliwahi kuhudumu katika jeshi la Marekani nchini Iraq.

Hayo yanajiri katika kipindi hiki ambapo kumeripotiwa kuongezeka chuki na ubaguzi dhidi ya Uislamu na Waislamu Marekani.

3505798

captcha