IQNA

Leo ni Arubaini ya Imam Husain AS, Waislamu wa Iran waungana na Waislamu wengine kuiadhimisha

11:48 - September 06, 2023
Habari ID: 3477555
Jumatano ya leo ya tarehe 6 Septemba 2023 inasadifiana na maombolezo ya Arubaini ya Imam Husain AS, yaani siku ya 40 tangu Imam Husain AS na wafuasi wake watiifu walipouawa kinyama kwenye jangwa la Karbala mwezi 10 Mfunguo Nne Muharram, mwaka wa 61 Hijria.

Imam Husain AS ni Imam wa Tatu katika kizazi kitoharifu cha Bwana Mtume Muhammad SAW na mamilioni ya Waislamu na wapenzi wa Ahlul Bayt AS wamekusanyika hivi sasa mjini Karbala Iraq kwa ajili ya kumbukumbu hizo.

Wafanya ziara kutoka kona zote za dunia wakiwemo wale wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wanaikumbuka kwa hamasa kubwa siku hii na kila mwaka wanaitumia siku hii kula kiapo cha kuendeleza njia tukufu ya Imam Husain AS ambayo ndiyo njia ya Bwana Mtume Muhammad SAW na ndiyo njia ya Uislamu halisi.

Muda wote wa safari yake ya kutoka Makkah kuelekea Karbala, Imam Husain AS alikuwa akisisitiza mara kwa mara kwamba ametoka kwa ajili ya kuinusuru dini ya Allah, kwa ajili ya kuwafedhehesha watawala waliokuwa wanatawala kinyume na mafundisho ya Uislamu na kwa ajili ya kuamrisha mema na kukataza mabaya. Kusimama dhidi ya dhulma na ukandamiza na kwa ajili ya kulinda Qur'ani Tukufu na kuibakisha hai dini tukufu ya Uislamu kama ilivyoletwa na Mtume Muhammad SAW.

Wananchi wa Iran kila mwaka wanaungana na Waislamu wengine duniani kuhudhuria kwenye misikiti na Husainia kwa ajili ya kuadhimisha siku hiyo.

Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inatoa mkono wa pole kwa Waislamu wote na kila mpenda haki duniani kwa mnasaba wa kumbukumbu ya Arubaini ya Imam Husain AS.

Kishikizo: imam hussein as
captcha