IQNA

Muuaji wa Waislamu New Zealand adai hana hatia

21:47 - June 14, 2019
Habari ID: 3472001
TEHRAN (IQNA) – Gaidi wa Australia aliyetekeleza mauaji ya Waislamu 51 katika misikiti miwili mjini Christchurch nchini New Zealand mwezi Machi ameiambia mahakama kuwa hana hatia.

Katika hujuma aliyoitangaza moja kwa moja kupitia Facebook, gaidi huyo wa Australia alitumia bunduki ya rashasha kuwashambulia Waislamu waliokuwa wakiswali Sala ya Ijumaa katika misikiti miwili mjini Christchurch mnamo Machi 15 mwaka huu.

Katika kesi iliyosikilizwa Ijumaa hii katika Mahakama Kuu ya Christchurch, gaidi Brenton Tarrant alikaa kimya  na kumsikiliza wakili wake, Shane Tait akizungumza kwa niaba yake na kutamka kuwa mteja wake hana hatia.

Hii ni kesi ya kwanza ya ugaidi kuwahi kusikilizwa nchini New Zealand.

Gaidi Tarrant binafsi hakufika mahakamani lakini alifuatilia kesi mubashara kwa njia ya video akiwa katika gereza ya Auckland.

Gaidi huyo anakabiliwa na mashtaka 51 ya mauaji, 40 ya jaribio la mauaji na kuhusika katika kitendo cha ugaidi. Jaji Cameron Mander amesema kesi hiyo itaanza Mei 4 mwakani na gaidi huyo ataendelea kubakia rumande.

Gaidi Tarrant ana misimamo mikali ya kibaguzi ya wazungu wanaoamini kuwa wazungu ndio kaumu bora zaidi na ni mfuasi sugu wa  Rais Donald Trump wa Marekani ambaye ni mashuhuri kwa chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu.

3819189

captcha