Wiki iliyopita Marekani ilitangaza itashirikiana na Bahrain kuwa mwenyeji wa kongamano litakalofanyika Juni 25-26 katika mji wa Manama kwa lengo eti la kuhimiza uwekezaji katika eneo linalokaliwa kwa mabavu la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Ukanda wa Ghaza ambao nao uko chini ya mzingiro.
Hatahivyo maafisa wa Palestina wanasema lengo kuu la kongamano hilo ni kuandaa mazingira ya utawala wa Rais Trump wa Marekani kuzindua kile ambacho kinatajwa kuwa ni 'Muamala wa Karne."
Katika taarifa Kamati ya Utendaji ya PLO imesema: "PLO inasisitiza msimamo wake wa mwisho wa kupinga kongamano hilo na haijatuma upande wowote kufanya mazungumzo kwa niaba ya watu wa Palestina."
Taarifa hiyo imeongeza kuwa lengo la Marekani katika kongamano hilo ni kuanza kutekeleza mpango wa 'Muamala wa Karne na kuunganisha na uchumi baada ya kuchukua hatua za kutekeleza upande wa kisiasa wa mpango huo.
PLO imesema 'muamala wa karne' unalenga kuuimarisha utawala wa Kizayuni wa Israel ambao unakaliwa kwa mabavu ardhi za Palestina na kufuta haki zote za kitaifa na kisheria za watu wa Palestina.
PLO imesisitiza kuhusu kupinga kikamilifu mpango huo tata wa Marekani na kusema itafungamana na haki za kisheria za Wapalestina.
Harakati ya Jihad Islami ya Palestina pia nayo imekosoa vikali mpango wa kufanyika mkutano wa Marekani wa kuzindua hatua ya mwanzo ya utekelezaji wa 'Muamala wa Karne' mwezi ujao wa Juni nchini Bahrain ikisisitiza kuwa kongamano hilo halina lengo jingine ghairi ya kuandaa mazingira ya kuimarisha na kufanya wa kawaida uhusiano kati ya Waarabu na utawala wa Kizayuni wa Israel.