IQNA

Barham Salih achaguliwa kuwa Rais mpya wa Iraq

17:52 - October 03, 2018
Habari ID: 3471700
TEHRAN (IQNA)-Jana Jumanne, Bunge la Iraq lilimchagua Barham Salih, kuwa rais mpya na Adil Abdul Mahdi kuwa waziri mkuu mpya wa nchi hiyo.

Kabla ya hapo, tarehe 15 ya mwezi uliopita wa Septemba bunge hilo lilimchagua Muhammad al-Halbousi kuwa spika mpya wa bunge. Tangu mwaka 2003 hadi sasa, na kwa mujibu wa mwafaka uliofikiwa kati ya makundi ya kisiasa ya Iraq, rais anachaguliwa miongoni mwa Wakurdi, spika wa bunge anatokana na wagombea wanaopendekezwa na Masuni na waziri mkuu anachaguliwa miongoni mwa Mashia.
Kuchaguliwa rais ni hatua ya kwanza katika uundaji wa serikali mpya ya Iraq. Kwa kuzingatia nukta hiyo, hatua ya mwanzo aliyochukua Rais Barham Salih baada ya kuchaguliwa hapo jana ilikuwa ni kumtambulisha Adil Abdul Mahdi kuwa Waziri Mkuu na kumtaka awe ameshatangaza baraza lake jipya la mawaziri ndani ya muda wa mwezi mmoja.
Kuchaguliwa Barham Salih kuwa rais mpya wa Iraq kuna umuhimu kwa sababu mwanasiasa huyo anafadhilisha na kutanguliza mbele maslahi ya taifa ya Iraq kuliko maslahi ya mirengo na matapo. Barham Salih, ambaye ni mgombea aliyependekezwa na chama cha Muungano wa Kizalendo wa Kurdistan (PUK), wakati ilipoitishwa kura ya maoni ya kutaka Kurdistan ijitenge na Iraq, yeye hakuunga mkono kura hiyo ya maoni na akataka kulindwa umoja wa ardhi yote ya Iraq. Hapo jana pia baada ya kutangazwa kuwa rais mpya wa Iraq, Barham Salih alisema, ataulinda umoja na kujitawala kwa Iraq. Alisisitiza pia kwa kusema: Nitakuwa rais wa Iraq, si wa kundi au mrengo maalumu. Tunaweza kusema kwamba moja ya ujumbe muhimu zaidi wa kuchaguliwa Barham Salih kuwa rais mpya wa Iraq ni kushindwa wale wanaotaka kujitenga na Iraq.
Umuhimu mwengine wa kuchaguliwa Barham Salih kuwa rais mpya wa Iraq ni kwamba yeye ni mtu mwenye uhusiano mzuri na Waarabu wa nchi hiyo; na hata kuchaguliwa kwake kwa kura 219 katika kikao cha jana cha bunge kumetokana na suala hilo. Kinyume na mtazamo wa baadhi ya shakhsia wengine maarufu wa Kikurdi, Barham Salih anaamini kwamba haki za Wakurdi zitapatikana katika "Iraq imara" na si "Iraq dhaifu".
Kutangazwa Adel Abdul Mahdi kuwa waziri mkuu mpya wa Iraq nako pia kumebeba ujumbe umhimu; nao ni kwamba mashinikizo ya nje ya kuchochea hitilafu baina ya makundi ya Kishia na pia kutaka kumpendekeza waziri mkuu anayeipinga harakati ya mapambano ya Kiislamu au Muqawama ya nchi hiyo ya Alhashdu-Sha'abi yamegonga mwamba, kwa sababu Adel Abdul Mahdi amechaguliwa kuwa waziri mkuu kupitia muungano wa makundi ya Kishia yaliyounda mrengo mkubwa kabisa bungeni kupitia mwafaka uliofikiwa kati ya mrengo wa Saairun na Al-Fat'h.

3466890

captcha