IQNA

Masharti kwa Washiriki wa Mashindano ya Kimataifa ya Qurani ya Walemavu wa Macho Iran

14:08 - September 04, 2018
Habari ID: 3471659
TEHRAN (IQNA) –Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetangaza masharti kwa wale wanaotaka kushiriki katika Duru ya 4 ya Mashindano ya Kimataifa ya Qur'ani ya Walemavu wa Macho.

Katika taarifa, Shirika la Hifadhi ya Kijamii Iran ambalo linaandaa mashindano hayo limesema wanaotaka kushiriki wana hadi Januari 21, 2019 kujisajili ili washiriki katika mashindano hayo ambayo yanatazamiwa kufanyika baada ya mwezi Machi mwaka huo huo.

Kati ya malengo ya mashindano hayo ni kuimarisha umoja na mashikamano wa Waislamu duniani, kuandaa jukwaa la kubadilishana mawazo ya kiutamaduni na kielimu baina ya washiriki, kustawisha utamaduni na mafundisho ya Qur'ani, kuwahimiza wenye ulemavu wa macho kustawisha maarifa yao ya Qur'ani na pia kuwaandalia washiriki harakati mbali mbali zinazohusiana na Qur'ani.

Kati ya masharti ya washiriki ni kuwa,  wawe na umri wa kuanzia miaka 18-45. Mashindano hayo ni ya wanaume pekee katika kategoria za kusoma na kuhifadhi Qur'ani Tukufu na kila mshiriki anaweza kushiriki tu katika kategoria moja. Aidha mshiriki anapaswa kuwa raia wa nchi ambayo anaiwakilisha. Halikadhalika wale walioshika nafasi ya kwanza hadi ya tatu katika mashindano yaliyopita hawawezi kushiriki katika mashindano yam waka huu.

Wanaotaka kushiriki wanaweza kuwasiliana na ofisi za Kituo cha Utamaduni cha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika nchi zao na kurekodi sauti zao au mwambata wa utamaduni wa Iran afike katika sehemu waliko ili kurekodi sauti zao na kisha kuzituma kwa njia ya email kupitia anuani ya hosseinse@gmail.com

Washiriki katika mashindano haya pia wanapaswa kuwa wameshika nafasi za kwanza katika mashindano yao ya kitaifa au ya kimataifa katika nchi zingine duniani na waweza na uwezo wa kuzingatia kanuni zote za usomaji Qur'ani na uwezo wa kujibu maswali haraka kwa wale wanaoshiriki katika kategoria ya kuhifadhi. Halikadhalika washiri wanapaswa kuwa na barua kutoka taasisi ya Kiislamu yenye itibari katika nchi yao yenye kuthibitisha kuwa wana uwezo wa kushiriki katika mashindano ya Qur'ani kwa mujibu wa masharti yaliyotajwa.

Duru ya 3 ya Mashindano ya Kimataifa ya Qur'ani ya Walemavu wa Macho ilifanyika katika mji mkuu wa Iran, Tehran mwaka huu sambamba na mashindano kadhaa ya Qur'ani yakiwemo Mashindano ya 35 ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu ya Iran.

3743797/

captcha