IQNA

Wanandoa Waislamu wanyimwa uraia wa Uswisi kwa kupinga kupeana mkono na ajinabi

15:08 - August 18, 2018
Habari ID: 3471633
TEHRAN (IQNA)- Mji wa Lausanne nchini Usiwisi umewazuia wanandoa Waislamu kuchukua uraia wa nchi hiyo kutokana na msimamo wao wa kukata kupeana mkono na watu ajinabi.

Meya wa Lusanne Gregoire Junod amesema manispaa yake imekataa kuwapa uraia wanandoa hao kutokana na kile alichodai kuwa ni msimamo wao wa kutoheshimu usawa wa kijinsia.

Meya huyo hakutaja majina au asili ya wanandoa hao lakini alisema walikataa kata kata kupeana mkono na watu wa jinsia mkabala. Junod amedai kuwa uhuru wa Imani na Dini unatambuliwa katika sheria za eneo hilo lakini akasema itikadi za kidini zinapaswa kuwa kwa mujibu wa sheria. Wanandoa hao wana siku 30 kukata rufaa kufuatia uamuzi huo.

Mwaka 2016 serikali ya Uswisi ilisitisha mchakato wa kuzipa uraia familia mbili za Waislamu ambao watoto wao wawili wa kiume mabarobaro walikataa kuwapa mikono walimu wao wa kike.

Ndugu hao wawili, ambao wakati huo walikuwa na umri wa miaka 14 na 15 , waliibua mjadala mkali Usiwisi kwa hatua yao hiyo ambayo inaenda sambamba na mafundisho ya Kiislamu.

Kwa mujibu wa mafundisho ya Kiislamu ni harami mwanamke Mwislamu kumpa mkono mwanaume ajnabi kama ambavyo mwanaume Mwislamu haruhusiwi kumpa mkono mwanamke ajnabi.

Aidha katika hatua nyingine yenye chuki dhidi ya Waislamu, mwaka 2009 asilimia 57 ya wananchi wa Uswisi walishawishiwa kwa propaganda chafu za chuki dhidi ya Uislamu kuunga mkono marufuku ya ujenzi wa minara katika misikiti nchini humo kupitia kura ya maoni. Kuna karibu Waislamu nusu milioni kati ya watu milioni 7 nchini Uswisi.

3466544

captcha